9/1/16

Mwalimu atozwa Sh800,000 kwa utumishi hewa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imemtoza faini ya Sh800,000 mwalimu wa Shule ya Sekondari Msalala, Henry Tagata kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh9 milioni kwa kupokea mishahara akiwa hayupo kwenye kituo chake cha kazi.


Mshtakiwa huyo alilipa kiasi hicho cha fedha na kunusurika kutumikia kifungo cha miaka mwili jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ushindi Swalo alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na waendesha mashtaka wa Takukuru juzi, Kelvin Mrusuri na Agustino Mtaki umethibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.


Ilidaiwa mahakamani hapo na Mrusuri kuwa Agosti, 2010 hadi Aprili, 2014, mshtakiwa akiwa mwalimu wa shule hiyo alitoweka kwenye kituo chake cha kazi na kuendelea kupokea mshahara na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya fedha hizo.


Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo akiwa ni mtumishi hewa, aliisababishia Serikali hasara kinyume na aya ya 10(1) jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa kupokea malipo ya mshahara asiyo stahili kwa kipindi ambacho hayuko kazini.


Katika shauri hilo namba sita ya mwaka 2016 la uhujumu uchumi, mshtakiwa alitakiwa kurejesha fedha za Serikali alizopokea kama mshahara akiwa hayuko kazini.


Hakimu Swalo alidai mahakamani hapo kuwa ametoa adhabu ya kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya Sh800,00 ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama ya mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo alilipa faini hiyo na kuachiwa huru. 
 
-Mwananchi
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts