Ndalichako Ahimiza Wasomi Kujiajiri | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

9/6/16

Ndalichako Ahimiza Wasomi KujiajiriWAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amewataka vijana waliopo masomoni na wahitimu nchini, kuhakikisha wanajifunza zaidi mbinu za kujiajiri na si kusubiri kuajiriwa.

Aidha Waziri huyo, ametoa changamoto kwa taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu kuzalisha wahitimu wenye taaluma na mikakati itakayowezesha kujiajiri na si wahitimu wanaotafuta ajira.

Aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Nicholaus Burreta wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Vijana, linalohusu mikakati ya kumaliza tatizo la ajira na rushwa.

“Ni kweli tatizo la rushwa ni kubwa si hapa nchini bali Afrika nzima kwa ujumla. Afrika ina watu takribani bilioni moja lakini kati yao milioni 50 hawana ajira. Nawapongeza vijana kwa kuliona hili na kuamua kulivalia njuga ili kulipatia ufumbuzi,” alisema.

Alisema wakati dawa ya ukosefu wa ajira ikiendelea kutafutwa duniani kote, ni wakati sasa kwa vijana wa kitanzania kuwa na mabadiliko ya kifikra na pindi wanapohitimu wajitahidi kuwa na elimu ya ziada itayowawezesha kujiajiri na si kusubiri ajira.

“Nasema tuachane na wasomi wanaosubiri ajira, hata taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu tutengeneze vijana wenye mitazamo chanya ya kujiajiri wenyewe. Hili si tu litawakwamua kiuchumi lakini pia litaongezea na kulijenga taifa kiuchumi,” alisema.

Alisema hali ya kuendelea kutoa elimu inayowafanya vijana wategemee zaidi kuajiriwa ndio inayochangia kuwepo na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi ambao matokeo yake huishia vijiweni.

Akizungumzia tatizo la rushwa, alisema tatizo hilo pamoja na kuendelea kutafuna nchi pia limekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa utawala bora katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.

Alisema tumaini la nchi yoyote ile ni vijana hivyo ni vyema taasisi husika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikaanza kushirikisha kwa ukaribu zaidi vijana katika kudhibiti vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake, Burreta alisema anaamini kuwa njia pekee itakayosaidia katika kupambana na tatizo la rushwa si kuwapatia maslahi bora watumishi wa umma au wafanyakazi tu bali ni kuwabadili mtazamo wao ili waichukie kabisa rushwa.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana (AYLTS), Nesia Malunje, alisema mkutano huo umewakutanisha vijana kutoka nchi 14 za Afrika baadhi yake ni Rwanda, Uganda na Sudan Kusini kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi dhidi ya matatizo ya ukosefu wa ajira na rushwa.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Umoja wa Mataifa, Stella Vuzzo, alisema uamuzi huo wa vijana kukutana na kuzungumzia matatizo ya ajira na rushwa ni muhimu kwani unaendana na malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayotekelezwa na nchi takribani 193 wanachama wa UN ikiwemo Tanzania.

Awali, akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu hali ya ajira kwa vijana nchini Tanzania, Meneja Utafiti kutoka AYLTS, Elizabeth Nkanda, alisema matokeo ya utafiti huo uliowahoji vijana takribani 3,000 nchi nzima yanaonesha kuwa asilimia 78 wanalalamikia tatizo la ukosefu wa ajira na rushwa.

google+

linkedin