Contact us: yuvinusm45@gmail.com | email: yuvinusm45@gmail.com

We're Coming Soon

Tutarudi Baada ya Matengenezo

Tupo kwenye matengenezo ya Mtandao Wetu Tutarudi Mchakato Ukishakamilika, Tunaomba Radhi kwa Usumbufu Utakaojitokeza!

We are working very hard on the new version of our site. It will bring a lot of new features. Stay tuned!


days

hours

minutes

seconds

Subscribe to our newsletter

Sign up now to our newsletter and you'll be one of the first to know when the site is ready:

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger
Design by Yuvinusm

9/1/16

Samia: Iwe kampeni ya kitaifa wasichana kusoma Sayansi
“NILIPOAMBIWA nije kufungua kongamano la wahandisi wanawake, picha niliyokuwa nayo ni kwamba nitakuta wahandisi ‘majimama’. Lakini nimeshangaa nilipoingia kwenye ukumbi, wengi wa niliowaona ni warembo. Kumbe inawezekana ukawa mhandisi, ukawa mrembo,” anasema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan huku akishangiliwa.

Kauli hiyo ya Makamu wa Rais ambayo iliibua kicheko sambamba na makofi ya nguvu kutoka kwa wahandisi hao aliitoa kwenye ufunguzi wa kongamano na maonesho ya wahandisi wanawake liliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam. Kongamano hilo lililoandaliwa na Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania lilihudhuriwa na wahandisi wanawake waliobobea, wanataaluma, wahitimu wa vyuo vikuu na wanafunzi wa kike kutoka baadhi ya shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam.

Kongamano hilo lilibeba kaulimbiu inayosema: “Kumwezesha mhandisi mwanamke kukuza ujuzi katika fani ya uhandisi ni kuchangia maendeleo ya jamii.” Kaulimbiu hiyo imekuja wakati mwafaka katika kipindi hiki ambapo taifa linahitaji wahandisi wengi kwa ajili ya kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda. Aidha, kaulimbiu hiyo imekuja katika kipindi ambapo Taifa linahitaji pia kufanikisha lengo la kuhamasisha wanawake wahandisi kuzigundua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kujiendeleza katika fani ya uhandisi na kutatua changamoto zinazokabili jumuiya ya Watanzania.

Mwelekeo huo wa kaulimbiu kwenda na wakati umeonekana pia hata kwenye mada zilizowasilishwa na wahandisi wanawake zikijumuisha ukuaji katika fani ya uhandisi na changamoto zake, uvumbuzi na matumizi ya teknolojia, ujasiriamali na biashara; pamoja na utawala na uongozi. Pamoja na jitihada za ndani ya kitengo za kukumbushana wajibu wao kupitia mada za kitaaluma zinazotolewa kwenye makongamano kama hayo, lakini bado, sekta ya uhandisi ina changamoto ya kuwa na idadi ndogo ya wanawake wahandisi.

Kwa mujibu wa Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania (ERB), Steven Mlote, bodi hiyo ambayo ina wajibu wa kusimamia wahandisi nchini imeona changamoto hiyo ya kukosekana kwa uwiano wa kijinsi katika taaluma ya uhandisi. Hii inatokana na ukweli kwamba asilimia 92 ya wahandisi nchini ni wanaume na ni asilimia nane tu ya wahandisi wanawake. Mlote anasema mwelekeo huo unafanana tu na uliopo kwenye taasisi za mafunzo ya uhandisi ambapo inaonekana wanaume wanaosoma masomo ya uhandisi ni wengi zaidi kuliko wanawake.

“Hivi sasa, tuna wahandisi 17,122 waliosajiliwa ambapo kati ya hao wanawake ni 1,438 tu. Kati ya hao (1,438), ni wahandisi 13 tu (yaani asilimia 5) ambao ni wahandisi waliobobea, 329 (asilimia 8) ni wahandisi wataalamu na waliobaki 1,109 ni wahandisi waliohitimu mafunzo ya uhandisi kutoka katika vyuo mbalimbali nchini,” anadokeza Mlote. Hali hiyo anasema kwa hakika hairidhishi hata kidogo na kwamba kuna haja ya kufanya jitihada zaidi kuibadilisha ili hatimaye idadi ya wahandisi wanawake iweze kuongezeka.

Anasema inatakiwa kazi ambazo hapo awali tuliaminishwa kwamba ni kazi za wanaume zionekane pia zikifanywa na wanawake kwa uwiano ulio takribani sawa. Changamoto hiyo imepelekea Makamu wa Rais kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania kuandaa kampeni mbalimbali zitakazohamasisha na kuhimiza wanafunzi, hasa wa kike kujenga ari ya kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati kama hatua ya kuongeza maradufu wahandisi wanawake nchini.

“Udahili wa wanawake katika fani mbalimbali za kihandisi umebaki kuwa wa chini, hivyo basi kuna haja ya kuongeza ushawishi kwa watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati na kudahiliwa katika vyuo vinavyofundisha fani ya uhandisi,” anasema Makamu wa Rais Samia. Anasisitiza kwamba kampeni hiyo ni muhimu kwani itasaidia kuwaelimisha, kuwaunganisha na kuwaendeleza watoto wa kike na hivyo kuwawezesha kujitambua na kuthamini nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia fani za sayansi na teknolojia.

Anasema serikali kwa kutambua umuhimu huo wa wahandisi katika maendeleo ya nchi hususan katika sekta za nishati, madini, barabara, maji, uvuvi na kilimo imeendelea kuweka mipango madhubuti ya kuinua na kuimarisha fani ya uhandisi. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuongeza vyuo vya uhandisi kutoka kimoja miaka ya 1970 mpaka vyuo tisa kwa sasa na na pia imeendelea kuongeza maabara katika shule za umma ili kuwavutia wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya anaiomba Serikali ihakikishe inakamilisha mpango wa kuweka vifaa kwenye maabara za shule za sekondari kote nchini kama hatua ya kuwavutia wasichana wengi zaidi kusoma masomo ya Sayansi. Makamu wa Rais anasema hilo halina mjadala ukizingatia kwamba serikali imeamua masomo ya sayansi kuwa ya lazima kuanzia kidato cha tatu na hivyo itahakikisha maabara shuleni zinakamilika pamoja na kuweka vifaa ili kuongeza ufanisi wa wataalamu nchini.

“Hapa, napenda kuzipongeza baadhi ya halmashauri nchini ambazo zimekamilisha ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na kuweka vifaa vyote vya kujifunzia, nataka niwahakikishie, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo kwa njia ya vitendo kwa wanafunzi,” anaeleza Makamu wa Rais. Jitihada hizo za kuongeza idadi ya wahandisi wanawake haziko kwa upande wa serikali peke yake, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Norway nchini ameileza hadhara hiyo, kuwa serikali yao itawasaidia wahandisi wanawake ili kuwawezesha na kunufaisha Taifa kiuchumi na kijamii.

Mlote anathibitisha ukweli huo na kusema Serikali ya Norway imekuwa ikisaidia sekta hiyo na kwamba mwezi uliopita Bodi imesaini mkataba mpya wa msaada wa jumla ya Sh bilioni 4.3 kwa ajili ya kuchangia mafunzo ya kitaaluma kwa wahandisi wanawake wapatao 150 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai, mwaka huu, kwenye maeneo yanayohusiana na mafuta na gesi.

Hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau wa maendeleo zinalenga katika kuhakikisha idadi ya wanawake inaongezeka kwenye upande wa taaluma ya uhandisi ili waweze kuikwamua nchi hii kutoka kwenye lindi la umasikini kwa sababu historia inaonesha wanawake wamekuwa waaminifu katika utendaji wao wa kazi. “Mheshimiwa Makamu wa Rais, wahandisi wanawake ni mradi, wakipewa kazi wanaifanya kwa uadilifu, kwa nidhamu na kwa weledi... Wangekuwa wengi nchi ingesonga mbele kwa haraka,” anaeleza Msajili Mlote huku akishangiliwa.

Makamu wa Rais pia ameliona hilo na kuwahakikishia wahandisi wanawake kuwa serikali, itatoa zabuni za kusimamia miradi ya kihandisi kwa wahandisi wa ndani wenye uzoefu na weledi hususan wanawake kwa kuwa ni waadilifu. “Kupitia wahandisi wetu wanawake, nchi yetu itakuwa na barabara bora, itakuwa na madaraja bora, miundombinu bora kwa ujumla wake. Mtakwenda kwa mwendo wa “Hapa Kazi Tu,” anaeleza Samia.

Makamu wa Rais anasema Seri kali ya Awamu ya Tano imewaweka wahandisi wengi tu kwenye serikali ikiamini wahandisi hao wazalendo hawatadanganywa kwa senti kidogo katika kuharibu baadhi ya miradi. “Tumetoa nafasi za kutosha kwa wahandisi, tumewaweka kwa kuwa tunawaamini hivyo mtuonyeshe imani hiyo, mwanamke ndiyo kila kitu, fani hii tulikuwa tunaiogopa, kuingia kwetu tumeinogesha, sijawahi kusikia mhandisi mwanamke kakamatwa, kafuja fedha za serikali, labda itokee tu kaingizwa bila yeye kujua,” anasema Samia.

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwaasa wahandisi wanawake kuhakikisha wanapendana, wanasaidiana na kuwasiliana kwa ajili ya kupeana fursa za kiuchumi zitakazopatikana hususan za ujasiriamali na vile vile wanashirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wahandisi wanaume bila kuwa tegemezi.

Ama kwa hakika lilikuwa ni kongamano la kufana sana kiasi ambacho Msajili wa Bodi aliwatia moyo kwa kusema ipo haja ya kupanua wigo wa ongezeko la wahandisi wanawake kwa kuwa na Msajili wa Bodi na Rais wa Chuo cha Taifa cha Teknolojia mwanamke ili kuwajengea uwezo na kuchochea wanawake wengi kujiunga na fani hiyo.