SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA. MAJIBU YA MASWALI NA HOJA ZA WADAU KWA MWEZI AGOSTI, 2016 | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

9/6/16

SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA. MAJIBU YA MASWALI NA HOJA ZA WADAU KWA MWEZI AGOSTI, 2016

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, inapenda kuwashukuru wadau na wananchi wote waliotuandikia maoni pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kwa kipindi cha mwezi Agosti, 2016. Tunapenda kuwajulisha wale wote waliotuandikia maoni na maswali na hawajafungua baruapepe zao (Emails) na kurasa zao za Facebook wazifungue kwani tumejibu kila swali na kuwatumia katika anwani husika na baadae kuyaunganisha maswali na maoni yanayofanana na kuyatolea majibu ya jumla kwa faida ya wasomaji wetu wengine ili kuendelea kuelimishana kuhusu masuala yanayohusu Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini.
1. Swali
Nawapongeza kwa kufanya kazi nzuri ya kuendesha mchakato wa ajira Tanzania, pili napenda kuuliza maswali mawili kama ifuatavyo, A. Napenda kujua ni vigezo vipi na ni kada gani ambayo huajiriwa kuwa Maafisa Mipango? B. je ni muda gani umebaki ili kuanza kutangaza Ajira?
Jibu
Tumepokea pongezi zako. Tukirudi katika maswali yako, nikianza na swali la kipengele A. ambalo unapenda kufahamu ni vigezo vipi na kada gani huajiriwa kama Maafisa Mipango. Vigezo vya kukuwezesha kuajiriwa kama Afisa Mipango DRJ II kwa mujibu wa Waraka wa Maendeleo ya Utumishi NA. 3 wa Mwaka 2015, Nyongeza VII Muundo wa Utumishi wa Maafisa Mipango sifa za kuingilia moja kwa moja ni, Kuajiriwa wenye shahada /Stashahada ya juu ya Mipango kutoka vyuo vinavyotambuliwa na Serikali ambao wamejiimarisha katika mojawapo ya fani zifuatazo:
• Mipango ya Maendeleo ya Mikoa,
• Mipango ya Menejimenti ya Mazingira,
• Mipango ya Maendeleo ya Idadi ya Watu,
• Mipango ya Uwekezaji na Maendeleo ya Fedha,
• Mipango ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu,
• Menejimenti ya Mazingira na Maendeleo ya Miji, na
• Maendeleo ya Uchumi.
Swali la kipengele B. ambalo umeuliza ni muda gani umebaki ili kuanza kutangaza ajira, Kwa kuwa Serikali bado inaendelea kukamilisha zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa ni vyema tukaendelea kuvuta subira hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na kama mlivyoarifiwa awali juu ya kusitishwa kwa Ajira, vivyohivyo mtapewa taarifa rasmi na mamlaka zinazohusika za kuendelea kutoa nafasi za Ajira.
2. Swali
Habari yako kiongozi? natumaini u mzima wa afya na unaendelea vizuri na majukumu ya kulijenga Taifa. Nina maswali ambayo naamini utanipatia majibu.
Je, endapo kijana amepata kazi serikalini kwa kupitia Sekretarieti ya Ajira baada ya kupita usaili na kuripoti katika kituo chake cha kazi na amefanya kazi kwa muda wa miezi kadhaa ila tatizo limetokea yeye hajapendezwa na mazingira ya kazi kwa namna moja au nyingine, Je!
1. Anaruhusiwa kufanya usaili mwingine pale utakapo tangazwa na Sekretarieti ya Ajira?
2. Kuna utaratibu gani wa mtu kuomba kubadilishiwa taasisi moja kwenda nyingine yoyote na sekretarieti ya Ajira? baada ya yeye kuripoti kituo chake cha kazi.
Jibu
Asante kwa swali lako. Ni kweli inawezekana ukawa umeripoti na hujapendezwa na mazingira ya kazi kwa sababu moja au nyingine japokuwa Serikali imejitahidi sana kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kiasi kikubwa ikiwemo maeneo ya huduma za jamii, vitendea kazi, miundombinu na hata maslahi kwa watumishi wake yameimarishwa ili kuhakikisha watumishi wake wanaweza kwenda kufanya kazi mahali popote ndani ya nchi na kutoa huduma kwa jamii inayomzunguka kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu, ingekuwa vizuri pia kama ungeleza kwa nini hujapendezwa na mazingira husika ila tunachoweza kukuelimisha ni kwamba unaruhusiwa kuomba kazi Sekretarieti ya Ajira pindi itakapotangaza nafasi ya juu zaidi ya ile uliyonayo. Mfano wewe ni mchumi daraja la II na Serikali imetangaza nafasi ya mchumi daraja la I ambayo itahitaji mtu mwenye uzoefu wa kazi (utendaji mzuri katika fani yake) kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu (3), hivyo endapo utakuwa na sifa/kigezo hicho unaweza kuomba na kushindanishwa na waombaji wengine ila ni lazima pia upitishe barua kwa mwajiri wako ili akuidhinishie kabla ya kuwasilisha maombi yako ya kazi.
Aidha, utambue wazi huruhusiwi kuomba nafasi ya kazi inayolingana na nafasi uliyonayo kwa kuwa utakuwa unaziba kwa makusudi mwanya wa wale wanaotafuta kazi kukosa kutokana na wewe uliyonayo kutaka kubadilisha kwa kutaka kuchagua maeneo ya kufanyia kazi, pasipokujua Utumishi wa Umma ni kutumikia watanzania wote mahali popote iwe mjini au kijijini.
Vilevile, umeuliza kuhusu utaratibu gani wa mtu anaweza kutumia kuomba kubadilishiwa taasisi moja kwenda nyingine yoyote na Sekretarieti ya Ajira? Tunapenda kukufahamisha kwamba Sekretarieti ya Ajira haina utaratibu wa kumbadilishia mtu kituo cha kazi baada ya kupangiwa na kuripoti kazini, kwakuwa jukumu la Taasisi hii kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya waajiri wengine katika Utumishi wa Umma, ikisha kamilisha kazi hiyo na kukupangia kituo cha kazi na wewe kwenda kuripoti na kukamilisha zile taratibu za msingi na kuajiriwa mwenye uwezo wa kukuamisha kituo kimoja kwenda kingine ni Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kuwa ndio mwenye dhamana ya kusimamia watumishi wote. Anaweza kukuandikia barua ya uhamisho ukiomba kubadili kituo kutokana na sababu utakazotoa, nae atapima endapo zitakuwa za msingi atakuhamisha kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu kulingana na mahitaji na uwepo wa nafasi husika kule unakotaka kuhamia.
3. Swali
Hello, hongera sana kwa kazi nzuri mnayofaya ya kurahisisha mawasiliano kati ya Umma na Sekretarieti ya Ajira na katika Utumishi wa Umma. Mimi niliwahi kuajiriwa na Serikali ila Ajira yangu ilisitishwa kwa kuwa nilienda kusoma bila ya ruhusa ya mwajiri. Hivyo niliamua kuandika barua kwa lengo la kuajiriwa tena baada ya ajira ya awali kusitishwa, ambapo ningependa kujua ombi langu limefikia wapi tangu nilipowatumia barua mwezi Mei, mwaka 2015 kwakuwa sijapata majibu ya barua yangu hadi sasa, nitafurahi sana endapo ombi langu litapata majibu. nakutakia makujumu mema.
Jibu
Asante kwa swali lako pamoja na pongezi zimepokelewa. kuhusu majibu ya barua yako tumejaribu kufuatilia katika kumbukumbu zetu hatujaweza kuona nakala yoyote kutoka kwako na kwa kuwa hujaeleza ni wapi ulipoituma inakuwa vigumu kwetu kuweza kukupa majibu ya hatua iliyofikiwa, hivyo tunakushauri endapo una nakala au unaweza kuandika barua nyingine ielekeze kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Maana ofisi hiyo ndio yenye dhamana ya kushughulikia Watumishi wa Umma ambao ni waajiriwa tayari kutokana na maelezo yako Ajira yako ilisitishwa kutokana na kuonekana mtoro kazini kama ulivyobainisha ulienda kusoma bila ya kupata kibali kutoka kwa mwajiri wako.
4. Swali
Habari Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, poleni na kazi ya kujenga Taifa. Mimi ni kijana wa kiume na mkazi wa Mwanjelwa Mbeya na pia ni muhitimu Chuo Kikuu cha Jordan.
Kuhusu kusitishwa kwa ajira mpya, kwanza naweza sema Rais wetu alikuwa sahihi kusitisha Ajira kutokana na uwepo wa watumishi hewa, nilikuwa nataka niwambie kuwa muda unazidi kwenda na atujapata taarifa yoyote nini kinaendelea japo mlisema zoezi la kuhakiki watumishi hewa bado linaendelea lakini bado hamjasema mtamaliza lini, nikimaanisha tarehe na siku, ilihali vijana asilimia kubwa waliohitimu wameanza kukata tamaa wakiamni Ajira zaweza zisiwepo sababu hawajui kesho yao na kuna baadhi walishindwa kusaini mikataba kwenye Taasisi binafsi wakiwa na uhakika wa Ajira sasa muda unaenda wengi wao wapo nyumbani na wakiwa njia panda bila kujua pakwenda.
Maoni yangu ningewaomba mjitahidi kabla ya mwezi huu kuisha muwe mmesha toa taarifa kamili kuhusu ajira mpya, na kama zoezi la kuhakiki watumishi hewa limekua bado linahitaji muda mwingi mwambieni Mhe. Rais John Pombe Magufuli aruhusu Ajira hata kama ishu ya watumishi hewa bado, kwa hawa wahitimu mliopanga kuwaajiri waajirini kwa kuwatengea (folder) lao ambalo alita ingiliana na waliopo kazini na Rais alisema hata toa ajira mpya akimaanisha zoezi litakuwa gumu zaidi kwa kuongeza watumishi wapya waunganishwe na wazamani, na sina imani kama nyie wenye dhamana ya kuajiri kwamba hamuwezi teknologia ya kutenganisha waajiri wa zamani na wapya ilihali sasa hivi teknolojia imekua, jamani nchi kama Rwanda watushinde? najua Rais wetu yupo siliazi mpelekeni hata proposal jinsi ya kufanya namna gani mtatenga watumishi waliopo na wa zamani ili operation ya kucheki watumishi hewa iendelee na waajiriwa wapya waanze kazi.
Na sera ya Rais wetu ni hapa kazi tu na sasa hivi nikiangalia kuna upungufu wa watumishi kama Madaktari, Walimu na sekta nyingine zenye uhaba wa wafanyakazi na muda unazidi kwenda je sera ya hapa kazi tu itaendana wakati mahospitalini hakuna wafanyakazi wa kutosha, vijijini hakuna walimu wa kutosha, tena gepu la watumishi walio hewa bado lipo wazi, jamani jitahidini nimeandika haya kwa maendeleo ya nchi pamoja na kupunguza idadi ya wahitimu waliopo nyumbani kwa mwaka na miezi sasa huku tegemeo na walichosomea kinahuishwa kuajiriwa serikalini na ofisi ya TAMISEMI Naibu Waziri Suleiman Jafo alisema wametenga budget ya kuajiri Watumishi wapya 71,000, kwa niaba ya wahitimu wanaosubiri Ajira nategemea mawazo yangu yatafanyiwa kazi na kupata majibu sahihi kabla ya mwezi huu kuisha. Asanteni sana na kazi njema.
Jibu
Tunashukuru kwa swali lako pamoja na maelezo marefu tumeyaopokea, yataendelea kufanyiwa kazi kadri inavyowezekana. Aidha, Serikali imejitahidi kutoa taarifa ya hatua iliyofikia katika uhakiki wa watumishi hewa mara kwa mara hata wiki iliyopita Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alizungumza na Waandishi wa habari na kuelezea kuwa zoezi hilo liko katika hatua nzuri na kuzitaka baadhi ya taasisi ambazo bado hazijawasilisha taarifa zao za watumishi hewa ziwasilishe kabla ya tarehe 26 Agosti, 2016 ili taarifa hiyo iweze kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua zaidi.
Hivyo, ni vyema tukaendelea kuvuta subira ili kupisha mamlaka husika kuweza kuratibu zoezi hilo kwa ufanisi kutokana na unyeti wake kwa mustakabali wa Taifa hili. Mwisho, nimalizie kwa kukuelewesha kuwa Sekretarieti ya Ajira ina dhamana ya kuendesha mchakato wa ajira kwa niaba ya waajiri katika Utumishi wa Umma ila siyo inayosimamia zoezi la uhakiki wala haiwezi kuendesha mchakato wa ajira bila ya kupata kibali cha kufanya hivyo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kwa kuwa suala la Ajira lina miongozo yake, linahitaji bajeti, kutengwa nafasi kwa mujibu wa ikama. Hivyo tusubiri zoezi hilo likamilike na baada ya hapo taarifa rasmi kuhusu mchakato wa Ajira Serikalini itatolewa na Mamlaka zinazohusika.
5. Swali
Habari, mimi ni mkazi wa Arusha na ni Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma tangu mwaka 2014 katika fani ya Utalii, Ombi langu kwenu ni kutupunguzia sisi waombaji wa kazi gaharama za kusafisiri hadi Dar- es -salaam kwa gharama kubwa na kulala hotelini unatumia zaidi ya TZS150,000 na mwisho wa siku mtu unaambulia patupu. naomba muwe na zonal offices hata temporary tu mimi nilisha hudhuria interview zenu ambazo kiukweli sikuona sababu ya kuwepo kwa ofisi moja tu.
Kila kanda sasa hivi ina Vyuo Vikuu kwa hiyo kama ni sehemu ya kufanyia interview ipo Arusha tuna vyuo vingi Kilimanjaro na Tanga pia manake ofisi zinaweza kuwa Kilimanjaro ni bora waombaji waliochaguliwa interview wa kanda fulani wakalipa walao 10,000 kwa ajli ya kuhamisha ofisi kwa muda ili waweze kufanyiwa interview kwa mtu ambaye hana kazi afu unataka mtu asafiri kutoka labda muleba hadi dar tu afu pia hana ndugu na aje akose hiyo kazi inauma sana.
Ni matumaini yangu kwamba kwa ajira zinazosubiriwa mapema mwezi ujao Sekretarieti ya Ajira itafikiria hili suala.
Jibu
Tunashukuru kwa hoja yako. Ni kweli gharama ya msailiwa kutoka eneo moja kwenda lingine kwa ajili ya usaili ni kubwa. Hili Sekretarieti ya Ajira imeliona na imeweza kujitahidi mara kadhaa kusogeza huduma zake karibu na wadau pale bajeti iliporuhusu. Kwa kuwa imeshafanya saili kadhaa katika mikoa, nyingine kikanda na pale iliposhindwa kutokana na ufinyu wa bajeti ndio imekuwa ikifanyia Dar es Salaam. Tunakuahidi kuendelea kuhakikisha tunasogeza huduma zetu karibu na wadau kadri bajeti itakavyoruhusu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 06 Septemba, 2016.

google+

linkedin