9/1/16

Serikali kuhakiki matangazo ya tiba asilia

SERIKALI imewataka waganga wa tiba asili nchini kuhakikisha wanapata vibali kutoka Baraza la Tiba Asilia kabla ya kupeleka matangazo yao katika vyombo vya habari.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika jana.

Alisema kila mganga wa tiba hiyo anatakiwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu na kuachana na matangazo yasiyofaa na kuweka mabango ya ovyo barabarani.

“Ni muhimu waganga kuzingatia sheria kulinda afya na haki za watumiaji wa tiba asili. Pia matangazo ya tiba yanayotoka katika vyombo vya habari ni lazima yapate kibali cha Baraza la Tiba Asili na mbadala na atakayokwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Kama ilivyo kaulimbiu ya mwaka huu kwamba ‘Kanuni za Udhibiti wa bidhaa za tiba asili Kanda ya Afrika’, inalenga kutoa majukumu kwa waganga wa tiba hii na mamlaka za usimamizi kuratibu kanuni, kusajili na kudhibiti bidhaa zinazotumiwa katika huduma za tiba asili nchini,” alisema John.

Aliwataka waganga wa tiba asili kujiepusha na migongano katika jamii kwa kuhusisha ushirikina na uchawi kama chanzo cha ugonjwa na kutoa elimu kwa umma kuhusu mkanganyiko huo.

“Mnatakiwa kuepuka matangazo yanayokinzana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa pamoja na matangazo ya dawa ambazo hazijafanyiwa uthibitisho kuwa salama,” alisema John.
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm