9/19/16

Studio Mpya ya Kurusha Bunge `laivu’ Yazua Utata


WAKATI vituo vya televisheni vimezuiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja (live) ya vikao vya Bunge kutokana na kuanzishwa kwa studio maalum ya chombo hicho cha kutunga sheria, uongozi wa Bunge umekiri kuwapo kwa hitilafu kwenye kituo hicho kunakosababisha kushindwa kurushwa kwa matangazo yake.
Vituo vya televisheni nchini vilizuiwa kurusha moja kwa moja matangazo ya bunge kutokana na kile kilichoelezwa Aprili 18, mwaka huu na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah kuwa jukumu la kurusha matangazo hayo litafanywa na chombo hicho chenyewe.
Dk. Kashilillah alisema siku hiyo kuwa kamera na vipaza sauti vya vyombo vya habari vya kielektroniki havitaruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge kwa lengo la kurekodi yanayoendelea.
Badala yake, alisema jukumu hilo litafanywa na bunge lenyewe kupitia 'feeder' maalum ili kurahisisha kila kituo cha redio na runinga kupata matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga mitambo yao bungeni.
Wakati uongozi wa Bunge ukiendelea na msimamo wake wa vikao vyake kutorushwa `live’, Nipashe imebaini kumekuwa na kukatika katika kwa matangazo ya moja kwa moja ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Aidha, kipindi cha kwanza cha 'Maswali kwa Waziri Mkuu' cha mkutano wa nne wa Bunge la 11 kilichofanyika Alhamisi , Septemba 8 mwaka huu, hakikurushwa moja kwa moja licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuulizwa maswali muhimu likiwamo la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kuhusu sintofahamu iliyokuwapo kuhusu kudorora kwa uchumi wa nchi.
Alipotafutwa na Nipashe bungeni mjini Dodoma Alhamisi ya wiki iliyopita, Dk. Kashilillah ndipo alipokiri kuwapo kwa hitilafu katika mitambo ya Bunge inayohusika na matangazo ya chombo hicho.
"Ni kweli, kumekuwa na kukatika katika kwa matangazo yetu. Sio kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu pekee, hata leo (Alhamisi iliyopita) yalikatika kutokana na hitilafu kwenye mitambo, wataalamu wetu wanaendelea kulishughulikia kwa kushirikiana na TBC," alisema Dk. Kashilillah.
Tangu kutolewa kwa zuio la waandishi wa runinga na redio kurekodi vikao vya Bunge moja kwa moja, kipindi cha maswali na majibu kinachofanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi na kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu ambacho hufanyika kila Alhamisi kwa nusu saa kuanzia saa 3:00 asubuhi siku ambazo kiongozi huyo wa shughuli za serikali bungeni anakuwepo, ndivyo hurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC).
Uamuzi wa kutorusha matangazo ya bunge moja kwa moja ulipingwa na kambi rasmi ya upinzani bungeni iliyoamua kususa vikao vya Bunge la Bajeti kuanzia Mei 30 hadi Juni 30, mwaka huu, ikitaja sababu kadhaa zikiwamo za kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na uamuzi wa kuwa na vikao 'bubu' vya mhimili huo.
Wabunge wa upinzani pia wamekuwa wakiulalamikia uongozi wa Bunge kwa uamuzi wa kuweka zuio kwa vyombo vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge wakidai watendaji wa studio ya Bunge wamekuwa wakichuja taarifa za kutoka bungeni wanazozigawa kwa vyombo vya habari.

Chanzo: Nipashe
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts