9/3/16

Vinara 500 ‘dili’ mishahara hewa sasa kuozea gerezani

HATIMAYE ile operesheni kabambe ya kuwabaini watumishi hewa katika idara za Serikali na taasisi mbalimbali za umma imeibua mshindo mkubwa baada ya maafisa zaidi ya 500 kubainika na orodha yao kuandaliwa ili wafikishwe mahakamani mmoja baada ya mwingine.
Hatua hiyo, ambayo huenda ikaishia kuwaweka gerezani baadhi yao kutumikia vifungo vya miaka mingi vinavyohusiana na makosa mbalimbali ya jinai pindi ikithibitika mahakamani, ni matokeo ya uchunguzi huo ulioiwezesha serikali kuwa na majina ya wahusika wote wa mipango hiyo haramu iliyokuwa ikinufaisha wachache huku ikiisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha katika kila mwisho wa mwezi.

Tangu kuingia madarakani, Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imekuwa ikipambana vikali dhidi ya vitendo vya ufisadi vikiwamo vya ulipaji wa mishahara kwa watumishi hewa wa umma.

Hadi kufikia mwezi uliopita, ilibainika kuwa kwa wastani, Serikali ilikuwa ikiingia hasara kwa kulipa mabilioni ya fedha katika kila mwezi kupitia malipo ya watumishi hewa.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk. Laurean Ndumbaro, alisema kuwa hadi kufikia jana, kazi ya uchunguzi iliyokuwa ikifanywa na vyombo mbalimbali ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikiendelea vizuri na kwamba tayari hatua mbalimbali za kisheria ziko mbioni kuchukuliwa baada ya kila kilichofanyika kujulikana kupitia uchunguzi huo wa kitaalamu.

“Wapo ambao wamefikishwa mahakamani kuhusikana na ulipaji wa mishahara hewa na wengine wanaendelea kuchunguzwa na Takukuru na wengine tumewachukulia hatua za kinidhamu,” alisema.

Akitoa ripoti ya watumishi hewa hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, alisema wamebaini watumishi hewa 16,127 nchi nzima ambao kwa mwezi walikuwa wakiigharimu serikali kiasi cha sh. bilioni 16.14.

Akizungumza na wakuu wa mikoa mara baada ya kuwaapisha Ikulu, Rais Magufuli aliwapa siku 15 kuhakikisha wanawaondoa watumishi hewa walio katika orodha ya malipo katika mikoa yao.

Baadhi ya wakuu wa mikoa walifanikiwa kuchunguza na kuwabaini watumishi hewa, lakini aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango, alifukuzwa kazi na Rais baada ya kudai mkoa wake hauna watumishi hewa.

Baada ya kufukuzwa na Rais Magufuli, uchunguzi ulifanyika kwenye mkoa huo na ilibainika wafanyakazi hewa 226.

Rais Magufuli aliwahi kumtaja mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwa alikuwa akijilipa mishahara hewa 17.

Nipashe ilifuatilia kujua hatma ya mtumishi huyo na kuambiwa kuwa tayari alishafukuzwa kazi na mamlaka hiyo baada ya kubainika kufanya ufisadi huo.

Habari kutoka ndani ya Mamlaka hiyo zilisema kuwa mfanyakazi huyo alikuwa ni wa Idara ya Uhasibu ya TRA lakini alishafukuzwa kazi siku nyingi zilizopita.

Chanzo cha kuaminika kutoka Makao Makuu ya TRA kilisema kuwa mfanyakazi huyo alifukuzwa kazi baada ya kubainika kujilipa mishahara hiyo katika akaunti yake.

Kilisema mfanyakazi huyo baada ya kuhojiwa alikiri kujilipa mishahara hiyo na ndipo alifukuzwa kazi.

“Huyu mfanyakazi alikuwa Idara ya Uhasibu… ni kweli alijilipa mishahara hiyo na baada ya kuhojiwa alikiri ndipo tukamfukuza kazi na kumpeleka mahakamani,” chanzo hicho kilieleza.

Rais Magufuli alimfichua mfanyakazi huyo alipokuwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, alipokuwa alihutubia kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais Oktoba 25, mwaka jana. 
 
chanzo: Nipashe
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts