9/20/16

Wadaiwa Vyuo Vikuu Kukiona, Watafutiwa Njia ya Kuwapata

BAADA ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kusumbuliwa kwa muda mrefu na wadaiwa sugu, sasa imeamua kutumia Mamlaka ya Mapato (TRA), kukamata wahitimu ambao wamejiajiri.
Mkurugenzi wa HESLB Abdulrazaq Badru (kushoto) akijadiliana jambo na Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Guardian, Wallece Maugo, na Mhariri Mkuu, wa The Guardian Ltd, Jese Kwayu.Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye ofisi za The Guardian Limited ambao ni wachapishaji wa Magazeti ya Nipashe, The Guardian na la michezo la Lete RAHA, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema watatumia pia Wakala wa Usajili na Utoaji wa Leseni za Biashara (BRELA), kuwatafuta wadaiwa hao.

“Kwa muda mrefu tumekuwa na changamoto ya kupata wanufaika wa mikopo ambao hawaingii kwenye sekta rasmi ya ajira, kwa sasa tuko kwenye mpango wa kutumia TRA na Brela kupata taarifa zao," alisema Badru.

“Hii ni kwasababu hawa wasio kwenye mfumo rasmi siyo kwamba ni maskini hawawezi kulipa, tatizo ni namna ya kuwapata, kwa hiyo kupitia taarifa za TRA tutajua kama wamefungua kampuni ama wana leseni ya biashara na wako wapi kwa sasa.

“Wapo baadhi ambao nawajua tena wanafedha kuliko sisi tulio kwenye ajira, mmoja alisikia anadaiwa akalipa deni lote hapohapo... akaenda na ofisini kwake akatafuta wafanyakazi wenye mkopo wa bodi akaahidi kuwalipia nusu kila mmoja na sehemu nyingine wajilipie wenyewe.”

Mbali na mfano wa mdaiwa huyo, Badru alisema kuna mhitimu mwingine ambaye baada ya masomo hakupata ajira hivyo akaajiriwa kuendesha bodaboda ya mtu na sasa amenunua yake na kila mwezi analipa bodi ya mikopo Sh. 100,000.

“Kwa hiyo sisi jambo la kwanza ni kuwapata wako wapi, na mfumo wa Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) ukikamilika kazi yetu ya kuwapata wadaiwa sugu itakuwa rahisi sana kwa sababu mfumo ule utakuwa na taarifa zote," Badru alisema.

“Sisi ni kupeleka tu majina mtu ukienda kuchukua Passport (hati ya kusafiria) wanajua unadaiwa, ukienda kukopa benki wanajua una mkopo mwingine wa benki.
"Hilo litarahisisha sana kazi yetu.”

Alisema kwa sasa bodi hiyo inadai Sh. bilioni 14 ambazo zilikopeshwa kwa wanafunzi mbalimbali kabla ya kuanzishwa kwa chombo hicho mwaka 2005.

Alisema kwa wakati huo, wanafunzi 38,000 walikopeshwa Sh. bilioni 51 na zaidi ya miaka 10 baadaye sasa, wamelipa Sh. bilioni 36.

Alisema baadhi ya wadaiwa hao, tayari majina yao yamepelekwa katika taasisi ya Credit Information Tanzania Limited ili ipeleke taarifa zao kwenye taasisi mbalimbali za kifedha zijue kwamba wanadaiwa.

“Tunataka kuhakikisha kwamba kwa miaka miwili ijayo tunakusanya fedha zote hizi, tukimaliza kukusanya hili deni lenye zaidi ya miaka 10 tunaweza kusema tuko vizuri,” alisema.

Alisema pia baada ya bodi hiyo kutangaza majina ya wadaiwa sugu kwenye magazeti na kueleza azma ya kuyapeleka Idara ya Uhamiaji ili wasiruhusiwe kusafiri nje, fedha zinazorudishwa kila mwezi zimeongezeka kutoka Sh. bilioni mbili kwa mwezi mpaka Sh. bilioni sita.

Mbali na kuzuiwa kusafiri nje ya nchi, HESLB pia ilielezea kusudio la kuhakikisha wadaiwa sugu hao wanazuiwa kokopa benki na kujiendeleza kimasoma ndani na nje ya nchi kupitia taasisi husika.

Aidha, Badru alisema badala ya kutangaza tu kwenye vyombo vya habari, wadaiwa watakaoendelea kukaidi kulipa fedha hizo sasa wataburuzwa mahakamani.

“Sheria mpya imetusaidia kutupa nguvu ya kupeleka wadaiwa wetu mahakamani na pia imesaidia fedha kulipwa haraka kwa sababu inataka sasa mwajiri akate mshahara wa mfanyakazi ambaye ni mdaiwa asilimia 10 badala ya nane ya awali,” alisema.

Alisema kwa mwajiri anayechelewa kupeleka fedha hizo bodi ndani ya siku 15 tangu azikate kwenye mshahara wa mfanyakazi wake ambaye ni mdaiwa wa HESLB, atatozwa pia faini ya asilimia 10.

“Mambo haya yanasaidia tupate fedha kwa wakati, na pia kiwango kilichokuwa kikikatwa ambacho ni cha chini licha ya kuongezeka kutoka asilimia nane mpaka 10, pia sasa kitakatwa mwanzo kabisa baada ya makato ya kodi ya serikali (paye) na ile ya mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema.

Kuhusu deni ambalo kwa sasa limeiva na wanufaika wanalilipa, Badru alisema ni Sh. bilioni 284 na tayari Sh. bilioni 105 zimelipwa.

“Hili ni lile linalotakiwa kila mnufaika aanze kulipa mwaka mmoja baada ya kuhitimu masomo yake, na jambo la msingi tunataka waone umuhimu wa kulipa hizi fedha ili wadogo wao pia waweze kukopa.” 
 
chanzo: Nipashe
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts