Walimu 13,000 wadai fedha zao za likizo, posho | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

9/15/16

Walimu 13,000 wadai fedha zao za likizo, posho


WALIMU 13,000 Zanzibar wanadai fedha za likizo na posho za masomo na kusababisha kiwango cha deni la walimu visiwani humo kufikia Sh. bilioni sita.
Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar (Zatu), Mussa Omar Tafurwa, alisema walimu visiwani humo wamekua wakipewa likizo bila ya kulipwa fedha za likizo.

Alisema pamoja na chama hicho kufuatilia tatizo hilo Wizara ya Elimu, lakini hakuna utekelezaji uliyofanyika na kusababisha malalamiko makubwa kutoka kwa wanachama wake.

“Kuna walimu wanashindwa kwenda kusalimia ndugu na jamaa zao kama unavyofahamu Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba akini wanapewa likizo bila ya kulipwa fedha ya likizo,” alisema.

Tafurwa alisema pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kufahamu tatizo hilo, lakini watendaji Wizara ya Elimu wamekuwa wazito kulimaliza na kusababisha baadhi ya walimu kwenda likizo bila ya malipo zaidi ya mara tatu.

“Kila mwalimu anatakiwa kulipwa fedha za likizo Sh. 100,000 pamoja na maslahi yake mengine, lakini wanalazimika kwenda likizo bila malipo,” alisema Tafurwa.

Alisema Rais Dk. Shein katika sherehe za wafanyakazi Mei Mosi, mwaka huu na katika uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi aligusia deni la walimu na kuahidi kushughulikia, lakini viongozi waliopewa dhamana na watendaji wameshindwa kulipatia ufumbuzi.

Alisema walimu wamekua wakifanya kazi katika mazingira magumu na hatua ya kutolipwa fedha zao za likizo kwa wakati muafaka kuna wavunja moyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wakati umefika serikali kuchunguza kwanini walimu hawalipwi fedha za likizo wakati ni haki yao pamoja na fedha wanapokuwa masomoni,” aliongeza kusema.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Hadija Bakar, alisema hayupo yatari kuzungumza tatizo hilo kwa njia ya simu baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi wake.

google+

linkedin