Wananchi wa Mkoa wa Kagera Watakiwa Kutobweteka na Kusubiri Misaada ya Serikali | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

9/18/16

Wananchi wa Mkoa wa Kagera Watakiwa Kutobweteka na Kusubiri Misaada ya Serikali


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amewataka wanasiasa nchini kutotumia kisiasa maafa ya Kagera yaliyotokana na tetemeko la ardhi na badala yake waungane kutoa misaada ya hali na mali kwa wathirika ambapo pia nchi za Kenya na Uganda zimekabidhi misaada yao.
Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa akimpa taarifa ya maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera na kuwataka wanasiasa nchini kutotumia maafa hayo kisiasa.
 
Aidha, rais ametoa onyo kwa watu wote wasiokuwa na mapenzi mema wanaotumia maafa hayo ya Kagera kukusanya fedha kutoka kwa watu mbalimbali na kuvitaka vyombo vya dola kuingia kazini na kuwakamata wahusika wote aliowaita matapeli.
 
Halikadhalika rais ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kutobweteka na kusubiri misaada ya serikali na kuwataka kujipanga kwa kufanya kazi na kwamba serikali itafanya yale yaliyo ndani ya uwezo wake.
 
Awali akitoa taarifa za maafa hayo yaliyotokana na tetemeko la ardhi jumamosi ya September 10 majira ya saa tisa alasiri waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa mbali na kuwashukuru wahisani na nchi rafiki waliotoa misaada yao pia amemueleza rais mahitaji makubwa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi waliokumbwa na maafa kuendelea na maisha yao ya kawaida.
 
Kabla ya waziri mkuu kuzungumza kaimu balozi wa Tanzania nchini Uganda balozi Elibariki Maleko amemkabidhi rais kiasi cha dola za kimarekani laki nne zilizotolewa na rais wa Uganda Mh Yoweri Kaguta Museveni kusaidia maafa hayo huku rais wa Kenya Mh Uhuru Kenyata akitoa mabati elfu nne, mablanketi mia nne na magodoro mia moja vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja kumi na tano.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya waziri mkuu tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 440 huku zaidi ya nyumba 480 zikibomolewa kabisa ambapo nyumba zaidi kumi na nne elfu na themanini zikipata nyufa na wananchi zaidi ya laki moja wakihitaji misaada.
 
-ITV
 

google+

linkedin