9/2/16

Ziara ya Rais Magufuli Pemba yazuia mkutano wa CUF

Image result for magufuli
Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli akianza ziara Zanzibar leo, Jeshi la Polisi limezuia mkutano wa CUF katika Wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Ziara ya Rais Magufuli ilithibitishwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa na itaanzia Pemba na kesho atakuwa Unguja. Hiyo ni ziara yake ya kwanza Zanzibar tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM, hivi karibuni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani Mohamed Shekhani alisema wameuzuia mkutano huo kwa kuwa uko jirani na uwanja unaotarajiwa kutumiwa na Rais Magufuli leo atakapohutubia mkutano wa hadhara.

Katibu wa CUF Wilaya ya Chake Chake, Saleh Nassor Juma alisema leo alitaka kufanya mkutano na waandishi wa habari kutoa tamko la kuunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lililowasimamisha uanachama viongozi 11 akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba.

“Niliwakatalia kwa hoja kwamba mkutano na waandishi wa habari ni haki yetu ya kikatiba na tulikwishawaarifu watu wa Idara ya Habari (Maelezo) juu ya kikao hicho halali ambacho wao pamoja na waandishi wa habari walituhakikishia wangehudhuria,” alisema katibu huyo.

Mmoja wa maofisa wa Idara ya Habari kisiwani Pemba ambaye hakupenda kutajwa jina alithibitisha kupokea amri ya polisi kuzuia mkutano huo.

“Tulikuwa tumeshajiandaa kwenda katika ‘press conference’ hiyo kabla ya kupokea taarifa ya kutaka tuchukue hatua hiyo,” alisema.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts