HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA (MB), NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA SHEREHE ZA UZINDUZI WA MKAKATI WA TAIFA WA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MIPANGO, DODOMA, TAREHE 19 OKTOBA 2016. | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

10/19/16

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA (MB), NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA SHEREHE ZA UZINDUZI WA MKAKATI WA TAIFA WA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MIPANGO, DODOMA, TAREHE 19 OKTOBA 2016.

 
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA (MB), NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA SHEREHE ZA UZINDUZI WA MKAKATI WA TAIFA WA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MIPANGO, DODOMA, TAREHE 19 OKTOBA 2016.

Mheshimiwa Jaffo Seleman Said (Mb), Naibu Waziri TAMISEMI

Dkt. Zainabu Chaula, Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI
Prof. Muhammad Bakari Kambi, Mganga Mkuu wa Serikali
Wakurugenzi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto,
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya,
Wakuu wa vitengo,
Wadau wa Maendeleo na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Wageni Waalikwa;
Wanahabari,
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukusanyika hapa siku ya leo. Pia, ninayo furaha kubwa kusimama mbele yenu kama mgeni rasmi katika kuzindua mkakati huu muhimu wa pili wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Pamoja na rasilimali chache tulizonazo, Tanzania imepiga hatua kidogo katika kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Mabibi na Mabwana,
Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana duniani na haswa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwemo. Utafiti uliofanyika na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani na Taasisi ya NIMR, ya viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza imeonyesha kuongezeka kwa viashiria hivyo. Idadi ya watu wanaovuta sigara ni asilimia 15.9%, wanaokunywa pombe ni asilimia 29.3%, wenye uzito uliopita kiasi 34.7%, shinikizo la damu ni asilimia 25.9% na wagonjwa wa kisukari ni asilimia 9.1%. Hii haikubaliki, na ni lazima tuongeze bidii katika kuyashughulikia.
Mkakati huu umekuja wakati muafaka, wakati tunatakiwa kutekeleza Mpango wa Malengo endelevu (Sustainable Development Goals) ambayo kati ya malengo kumi na saba, matatu yanazungumzia jinsi ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, baadhi ya malengo haya ni;
Kufikia mwaka 2030, kupunguza moja ya tatu ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kukinga, kutibu na kuzingatia afya ya akili;
Kuboresha huduma za kinga na tiba ya utumiaji wa madawa ya kulevya na pombe;
Kufikia mwaka 2020, kupunguza nusu ya idadi ya vifo duniani na ajali za barabarani.
Mabibi na Mabwana,
Napenda kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Chama cha kupambana na ugonjwa wa kisukari duniani (World Diabetes Foundation) na chama cha kisukari cha Tanzania (Tanzania Diabetes Association), kwa kuwezesha kupitiwa kwa mkakati wa zamani wa mwaka 2008-2015, na kutengenezwa huu wa sasa, ambao ni wa 2016-2020. Kwa kushirikiana na kitengo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, TDA imeweza kutekeleza mpango wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchi nzima.
Aidha nawashukuru kwa dhati wadau wetu wa Maendeleo kwa misaada mbalimbali ambayo imechangia katika kuboresha Afya za Watanzania.
Mabibi na Mabwana,
Ninayo taarifa kuwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya mmeombwa kuteua mtu mmoja atakayeratibu shughuli zote za magonjwa yasiyo ya kuambukiza mikoani na wilayani kwenu. Ni matarajio yangu kuwa mtafanya kazi kwa nguvu na kwa ukaribu zaidi na kitengo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza cha Wizara ili huduma hizi ziwafikie watu wote hadi ngazi ya jamii.
Baada ya kusema haya machache , sasa natamka kuwa Mkakati huu wa pili wa kitaifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza umezinduliwa rasmi.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

google+

linkedin

0 comments: