10/19/16

MAJIBU YA HOJA ZA WADAU KWA MWEZI SEPTEMBA, 2016 KUTOKA SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, inapenda kuwashukuru wadau na wananchi wote waliotuandikia maoni pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kwa kipindi cha mwezi Septemba, 2016.
Tunapenda kuwajulisha wale wote waliotuandikia maoni na maswali na hawajafungua barua pepe zao (Emails) na kurasa zao za “Facebook” wazifungue kwani tumejibu kila swali na kuwatumia katika anwani husika na baadae kuyaunganisha maswali na maoni yanayofanana na kuyatolea majibu ya jumla kwa faida ya wasomaji wetu wengine ili kuendelea kuelimishana kuhusu masuala yanayohusu Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini.
1.    Swali
Napenda kuuliza swali moja ambalo limekuwa likininyima usingizi kwa kuwa nataka kufahamu ni muda gani umebaki ili kuanza kutangaza Ajira maana niliwahi kumsikia mkuu wa nchi akisema mtachukua miezi miwili kufanya zoezi la uhakiki nayo imepita tunaona kimya je tuwaeleweje sisi watanzania wenzenu?
    Jibu
Awali ya yote tunashukuru kwa swali lako. Ni kweli mtakumbuka hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa ya kusitisha kwa muda Ajira mpya Serikalini kwa ajili ya kupisha zoezi la uhakiki wa Watumishi wake pamoja na zoezi la kupitia upya miundo yake, mazoezi haya mpaka sasa yanaendelea na hayajakamilika hivyo zoezi la usitishwaji wa Ajira bado linaendelea. Sekretarieti ya Ajira inapenda kuwajulisha kuwa pindi kazi hiyo itakapokamilika na kabla ya kuanza kutangaza itatoa taarifa ya kuanza kutangaza nafasi wazi za kazi kulingana na vibali vitakavyotolewa, hivyo inawaomba wananchi na wadau wote kuendelea kuvuta subira hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na kama mlivyoarifiwa awali juu ya kusitishwa kwa Ajira,  vivyo hivyo mtapewa taarifa rasmi na mamlaka zinazohusika za kuendelea kutoa nafasi za Ajira.

2.    Swali
Je, ni kweli Sekretarieti ya Ajira hamtoi vibali vya kuajiri kwa sasa hata kama Taasisi itapenda kuendesha mchakato wa ajira yenyewe?
    Jibu
Tunashukuru kwa swali lako. Napenda nikufahamishe kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ina jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma na haina mamlaka ya kutoa vibali vya ajira. Jukumu la kutoa vibali liko Menejimenti ya Utumishi wa Umma ndio wenye dhamana ya kufanya hivyo.

3. Swali
Mimi ni Mtanzania niko mkoani Kigoma sehemu ya Kasulu. nimeona mmetangaza nafasi za kazi zadi ya 1000 kupitia mitandao ya kijamii, sasa nilitaka kujua utaratibu wa kuwasilisha maombi ya nafasi hizo maana nimesomea masomo ya uhasibu na kuna nafasi ya mhasibu msaidizi katika hilo tangazo la nafasi za kazi.
    Jibu
Tunashukuru kwa swali lako. Ni kweli kuna tangazo la nafasi za kazi lililokuwa likidai Sekretarieti ya Ajira yatoa nafasi wazi za kazi  zaidi ya 1000. Napenda kukutaarifu kuwa tangazo hilo lililokuwa katika mitandao ya kijamii kuanzia tarehe 29 Septemba, 2016 halikutolewa na Sekretarieti ya Ajira kama mhusika /wahusika walivyodai.
Aidha, baada ya kuliona Sekretarieti ya Ajira haikukaa kimya bali kwa hatua za awali ilitolea taarifa ya kukanusha tarehe 30 Septemba, 2016 asubuhi na pia ilifanya Mkutano na Vyombo mbalimbali vya Habari tarehe 1 Oktoba mwaka huu ili kuendelea kukanusha na kutoa ufafanuzi juu ya tangazo hilo la uongo ambalo katika hali isiyokuwa ya kawaida mhusika/wahusika kwa utashi wao huku wakijua taarifa wanazosambaza ni za uongo walichukua matangazo yetu ya zamani na kuyafanyia marekebisho ya hapa na pale na katika tangazo hilo wamewataka watanzania wenye sifa na uwezo kujaza jumla ya nafasi wazi za kazi 1,101.
Taarifa hiyo ilikuwa imebainisha kuwa nafasi hizo ni kwa ajili ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii na Mtendaji Mkuu Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) licha ya kufahamu kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote, hali ambayo imeleta usumbufu kwa jamii na Serikali kwa ujumla.
Napenda kuendelea kukufahamisha mdau wetu na jamii kwa jumla kuwa aliyeanzisha uzushi huo alichukua matangazo ya mwaka jana yaliyotolewa na Sekretarieti ya Ajira tarehe 9 Julai, 2015 kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili yaliyokuwa na Kumb.Na. EA.7/96/01/H/56 ambayo yalikuwa na jumla ya nafasi za kazi 599 pamoja na tangazo lenye Kumb.Na. EA.7/96/01/H/57 lililokuwa na nafasi wazi za kazi 513. Mtu huyo mwenye dhamira mbaya baada ya kufanya  mabadiliko katika tarehe za kutangaza, huku akijua matangazo yote mawili yalikuwa yametolewa na Taasisi hii kwa niaba ya waajiri wanne tofauti ambao ni Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Aidha, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa Ajira na pia ushindani wa ajira nchini tangazo hili liliweza kusambaa kwa haraka hivyo kuweza kupotosha Umma kwa kiasi kikubwa hivyo Sekretarieti ya Ajira pamoja na kukanusha juu ya uvumi huu ili wananchi na wadau wetu muweze kuzipuuza pia tunaendelea kufuatilia vyanzo vya upotoshaji huu kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya dola ili kumbaini ama kuwabaini wale wote walioshiriki kufanya upotoshaji huu kwa jamii ili kuweza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria. 
Mwisho tunakuomba mdau wetu na watanzania kwa ujumla wanaotafuta kazi Serikalini kupitia Sekretarieti ya Ajira pindi wanapoona tangazo la nafasi za kazi mahali zinazodaiwa kutolewa na Taasisi hii kabla ya kuyafanyia kazi wajiridhishe kwanza kwa kufungua Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tz au portal ya Ajira ambayo ni portal.ajira.go.tz. ili kuepuka kutapeliwa au kuondokana na usumbufu usiokuwa na lazima.

4. Swali
Habari Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, poleni na kazi ya kujenga Taifa. Mimi ni kijana wa kiume  na mkazi wa Mwanjelwa Mbeya na pia ni muhitimu Chuo Kikuu cha Jordan.

Kuhusu kusitishwa kwa ajira mpya, kwanza naweza sema Rais wetu alikuwa sahihi kusitisha Ajira kutokana na uwepo wa watumishi hewa, nilikuwa nataka niwambie kuwa muda unazidi kwenda na atujapata taarifa yoyote nini kinaendelea japo mlisema zoezi la kuhakiki watumishi hewa bado linaendelea lakini bado hamjasema mtamaliza lini, nikimaanisha tarehe na siku, ilihali vijana asilimia kubwa waliohitimu wameanza kukata tamaa wakiamni Ajira zaweza zisiwepo sababu hawajui kesho yao na kuna baadhi walishindwa kusaini mikataba kwenye Taasisi binafsi wakiwa na uhakika wa Ajira sasa muda unaenda wengi wao wapo nyumbani na wakiwa njia panda bila kujua pakwenda.

Maoni yangu ningewaomba mjitahidi kabla ya mwezi huu kuisha muwe mmesha toa taarifa kamili kuhusu ajira mpya, na kama zoezi la kuhakiki watumishi hewa limekua bado linahitaji muda mwingi mwambieni Mhe. Rais John Pombe Magufuli aruhusu Ajira hata kama ishu ya watumishi hewa bado, kwa hawa wahitimu mliopanga kuwaajiri waajirini kwa kuwatengea (folder) lao ambalo alitaingiliana na waliopo kazini na Rais alisema hata toa ajira mpya akimaanisha zoezi litakuwa gumu zaidi kwa kuongeza watumishi wapya waunganishwe na wazamani, na sina imani kama nyie wenye dhamana ya kuajiri kwamba hamuwezi teknologia ya kutenganisha waajiri wa zamani na wapya ilihali sasa hivi teknolojia imekua, jamani nchi kama Rwanda watushinde? najua Rais wetu yupo siliazi mpelekeni hata proposal jinsi ya kufanya namna gani mtatenga watumishi waliopo na wa zamani ili operation ya kucheki watumishi hewa iendelee na waajiriwa wapya waanze kazi. Na  sera ya Rais wetu ni hapa kazi tu na sasa hivi nikiangalia kuna upungufu wa watumishi kama Madaktari, Walimu na sekta nyingine zenye uhaba wa wafanyakazi na muda unazidi kwenda je sera ya hapa kazi tu itaendana wakati mahospitalini hakuna wafanyakazi wa kutosha, vijijini hakuna walimu wa kutosha, tena gepu la watumishi walio hewa bado lipo wazi, jamani jitahidini nimeandika haya kwa maendeleo ya nchi pamoja na kupunguza idadi ya wahitimu waliopo nyumbani kwa mwaka na miezi sasa huku tegemeo na walichosomea kinahuishwa kuajiriwa serikalini na ofisi ya TAMISEMI Naibu Waziri Suleiman Jafo alisema wametenga budget ya kuajiri Watumishi wapya 71,000, kwa niaba ya wahitimu wanaosubiri Ajira nategemea mawazo yangu yatafanyiwa kazi na kupata majibu sahihi kabla ya mwezi huu kuisha. Asanteni sana na kazi njema.

    Jibu
Tunashukuru kwa swali lako ambalo ulilituma mwezi uliopita na sasa umelituma kwa mara nyingine pamoja na maelezo marefu tumeyapokea, yataendelea kufanyiwa kazi kadri inavyowezekana. Aidha, Serikali imejitahidi kutoa taarifa ya hatua iliyofikia katika uhakiki wa watumishi wake mara kwa mara hata hivi karibuni Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora nao walizungumza TBC1 katika kipindi cha ''TUNATEKELEZA'' juu ya hatua waliyofikia katika kutekeleza zoezi hilo la uhakiki ambalo liko katika hatua nzuri.
Hivyo, ni vyema tukaendelea kuvuta subira ili kupisha mamlaka husika kuweza kuratibu zoezi hilo kwa ufanisi kutokana na unyeti wake kwa mustakabali wa Taifa hili. Mwisho, nimalizie kwa kukufahamisha kuwa Sekretarieti ya Ajira imepewa dhamana ya kuendesha mchakato wa ajira kwa niaba ya waajiri katika Utumishi wa Umma ila siyo inayosimamia zoezi la uhakiki wa Watumishi Serikalini.
Ili Sekretarieti ya Ajira iweze kuendesha mchakato wa Ajira ni lazima kwanza ipate kibali cha kufanya hivyo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia kwa Waajiri husika waliokuwa wameomba kibali cha kuajiri kwa kuwa suala la Ajira Serikalini lina miongozo yake, ikiwemo kutengwa kwa  bajeti, kuainishwa kwa nafasi kwa mujibu wa ikama nk. Hivyo, nakushauri pamoja na wadau wengine tuendelee kusubiri zoezi hilo likamilike na baada ya hapo taarifa rasmi kuhusu kuanza tena kwa mchakato wa Ajira Serikalini itatolewa na Mamlaka zinazohusika.

5. Swali
Je, naweza kujua wajibu na vigezo ninavyopaswa kuzingatia kama Mwombaji wa nafasi za kazi katika Sekretarieti ya Ajira?
    Jibu
Tunashukuru kwa swali lako na majibu ya swali lako ni kama yalivyobainishwa hapa chini;
•    Wajibu wa mwombaji wa kazi/Ajira kwanza anapaswa kuzingatia nafasi za kazi zilizotangazwa katika Vyombo vya Habari kama vile Magazeti/ Radio/ Runinga na Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz au Tovuti za Wizara ama Taasisi husika zitakazokuwa zimetajwa katika tangazo husika. Aidha, Mwombaji wa kazi anatakiwa kusoma na  kuzingatia masharti ya Tangazo la kazi kama ifuatavyo:-
(i)    Tangazo la kazi ni la aina gani kwa kuangalia kada na vigezo husika (sifa za msingi za kazi husika).

(ii)    Uraia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila mwombaji anapaswa kuwa na cheti cha kuzaliwa.

(iii)    Mwombaji ambaye ni Mtumishi wa Umma ni lazima ajue kuwa kama anaomba kazi baada ya yeye kujiendeleza ni lazima apitishe barua yake kwa mwajiri ili kupata ridhaa ya Mwajiri, kutofanya hivyo kunamwondolea sifa ya kuomba kazi.

(iv)    Mwombaji ambaye tayari ni Mtumishi wa Umma na ameomba kazi ya Cheo cha juu ambayo imetangazwa katika Ofisi ya Serikali/ ama Taasisi za Umma ni lazima ajue kuwa anao wajibu wa kupitisha barua ya maombi kwa Mwajiri wake.

(v)    Mwombaji ambaye tayari ni Mtumishi wa Umma anapaswa kujua kuwa haruhusiwi kuomba tena nafasi ya kazi katika Utumishi wa Umma kwa nafasi ya kazi inayofanana na aliyoko kwa wakati huo. Mfano, Mtumishi ambaye ni Mchumi daraja la pili katika Wizara fulani na ameona tangazo linahitaji Mchumi daraja la pili katika Wizara nyingine haruhusiwi tena kuiomba kazi hiyo. Sababu ya msingi ya kuzuia ni kutokana na kuwepo kwa taratibu nyingine ambazo zitampa fursa pana Mtumishi wa aina hii ikiwemo uhamisho kwenda kwa Mwajiri mwingine.

(vi)    Mwombaji ajue kuwa anatakiwa anapoomba kazi aambatanishe na maelezo yake binafsi yaani (CV)

(vii)    Mwombaji katika maombi yake anatakiwa aambatanishe  pamoja na nakala ya Vyeti vya kuhitimu hatua mbalimbali za masomo.  Na nakala hizo ziwiane na maelezo aliyoyatoa katika maelezo binafsi (CV)

(viii)    Mwombaji anatakiwa kuweka picha ndogo ya “passport size” katika maombi yake.

•    Umri wa juu uliopo Kisheria ambao unamwezesha mwombaji kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu isizidi miaka 45. Ukomo wa umri umewekwa kisheria ili kumwezesha Mwombaji kuchangia mafao yake ya uzeeni kwa miaka 15, maana miaka 15 ndiyo kigezo cha kutimiza masharti ya kulipwa pensheni.  Aidha, kwa wale wenye umri wa zaidi ya miaka 45 wanaweza kuajiriwa kwa mkataba. Hata hivyo baadhi ya nafasi za kazi zinazotangazwa huwa na mahitaji yake maalum ya umri na uzoefu wa kazi husika.

•    Mwombaji anapaswa kujua kuwa endapo atakuwa amestaafu kazi, ameachishwa kazi, amepunguzwa kazi, amefukuzwa kazi, amestaafishwa kazi kwa manufaa ya umma haruhusiwi kuomba kazi Serikalini, mpaka apate kibali cha Mkuu wa Utumishi wa Umma.

•    Mwombaji anapaswa kujua kuwa endapo atawasilisha taarifa za kugushi atachukuliwa hatua za kisheria.

•    Mwombaji anapaswa kujua tarehe ya mwisho ya kuwasilisha  maombi kwa mujibu wa Tangazo.

•    Mwombaji wa kazi/ajira anatakiwa kuzingatia masharti ya jumla ya Tangazo kutofanya hivyo kunamnyima fursa ya kufikiriwa kuajiriwa Serikalini.

•    Mwombaji anapaswa kujua kuwa maombi yote kwa sasa yanatakiwa kutumwa kwa njia ya mtandao ambapo maelekezo ya namna ya kujisajili yapo kwenye tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz ataona namna ya kuingia kwenye portal ya Ajira kupitia anwani ''Recruitment Portal'' (portal.ajira.go.tz).
•    Mwombaji anapaswa katika barua yake ya maombi ya kazi  anwani aelekeze kwa Katibu, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, S.L.P. 63100 Dar es Salaam. Aidha, lengo la kufanya hivi ni kupunguza na hatimaye kuondoa uwezekano wa kuwasilisha barua kwa mkono na kuonana na Maafisa wa Sekretarieti ana kwa ana, malalamiko ya barua kuchelewa kuifikia Taasisi na wakati mwingine kupotea.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 17 Oktoba, 2016. Kwa maelezo zaidi, Piga 0687 624975, tuandikie au tutembelee katika Ofisi zetu kama anwani inayoonekana hapo chini;-

Ofisi ya Rais,
Sekretarierieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
27 Barabara ya Bibi Titi Mohamed,
S.L.P. 63100
Maktaba Kuu ya Taifa
11102 Dar es Salaam
Ghorofa ya pili, Jumatatu  hadi Ijumaa saa 1:30 asubuhi hadi 9:30 alasiri.
Share:
Post a Comment

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts